WAZIRI SILAA AKABIDHI MAGARI 16 KUTEKELEZA MRADI WA LTIP
Imewekwa: 22 Feb, 2024
WAZIRI SILAA AKABIDHI MAGARI 16 KUTEKELEZA MRADI WA LTIP

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa amekabidhi magari 16 yenye jumla ya Shilingi bilioni 2,079,852,965.54 ikizingatiwa gharama ya gari moja ni Shilingi 129,990,810.35 ambayo yatatumika kwenye Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa hapa nchini.

Waziri Silaa amesema hayo Februari 19, 2024 katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma wakati akikabidhi magari hayo kwa Katibu Mkuu ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga .

"Magari haya yatumike kwa kazi ya mradi, wale wote watakaokabidhiwa magari haya wayatumie vizuri, wayatunze. Napenda kuyaona yanafanyakazi na kuongeza kasi ya utekelezaji wa uboreshaji wa milki, kazi ya matumizi bora ya ardhi vijijini na kazi ya urasimishaji katika Halmashauri mijini" amesema Waziri Silaa.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga amesema Mradi huo unaotekelezwa nchini chini ya Wizara ya Adhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi unagharimu zaidi shilingi bilioni 346 ambazo ni sawa na dola za Kimarekani milioni 150. 

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) Bw. Joseph Shewiyo amesema mradi huo unajukumu la kusimamia usalama wa milki za ardhi mijini na vijijini ambapo amewahamasisha wanandoa wawe na umiliki wa ardhi wa pamoja.

Aidha, Bw. Shewiyo ameongeza kuwa mradi huo unatekelezwa katika Halmashauri 36, mitaa 660, vijiji 1700 na umetoa ajira kwa watumishi 700 ambao wanafanyakazi katika halmashauri hizo.

Mradi huo ni wa miaka mitano kuanzia 2022 hadi 2027 unatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Benki ya Dunia

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo