VIJIJI 52 MVOMERO KUNUFAIKA NA MRADI WA LTIP
Imewekwa: 23 Apr, 2024
VIJIJI 52 MVOMERO KUNUFAIKA NA MRADI WA LTIP

Vijiji takribani 52 katika Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro vitanufaika na Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) kwa kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Bw. Linno Pius Mwageni wakati wa kujadili utekelezaji wa Mradi huo katika ukumbi wa Halmashauri ya Mvomero, tarehe 22 Aprili 2024 Mkoani Morogoro.

Alisema kupitia mradi huu lengo ni kuandaa jumla ya Mipango Shirikishi ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji 52 katika Wilaya ya Mvomero ambapo hadi kufikia sasa tayari mipango 48 imekwishaandaliwa.  

‘‘Tarafa nne zilizopo Mvomero zitakazonufaika na mradi huu ni Tarafa ya Mgeta - vijiji 19, Tarafa ya Mvomero - vijiji 11, Tarafa ya Mlali - vijiji 11 na Tarafa ya Turiani - vijiji 11 ambavyo kwa pamoja vitakuwa na jumla ya mipango ya matumizi ya ardhi 52’’ alisema Mwageni.

Msimamizi wa Mradi katika Wilaya ya Mvomero Bw. Sambalu Simon amesema kuwa lengo la kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji ni kuimarisha milki za ardhi na matumizi yake, kugawa ardhi na kuboresha matumizi na hifadhi ya ardhi kulingana na mapendekezo na uwezo wa Kijiji, kubaini na kutenga maeneo ya umma pamoja na kuimarisha utunzaji wa mazingira kupitia sheria ndogo zinazotungwa kusimamia mpango.

Nae Bi. Sofia Lucas mkazi katika Wilaya ya Mvomero alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi huo Wilayani kwao, kwa kuwa mradi umewekeza sana katika kutoa elimu kwa jamii hususani makundi maalumu kama ushiriki wa wanawake katika kumiliki ardhi ili kuwakomboa kiuchumi.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umeweka nguvu kubwa katika kutoa elimu kwa wananchi kuanzia ngazi ya Kitaifa, Wilaya, Mtaa/Kijiji mpaka Kitongoji ikiwa ni pamoja na kuzingatia haki za makundi mbalimbali yakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wanawake, vijana, wenye ulemavu sambamba na utoaji wa elimu ya usawa wa jinsia katika umiliki wa Ardhi ili kuhakikisha usalama kwa kila kipande cha ardhi kwa Mtanzania.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo