Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) ni tumaini jipya la kuwainua kiuchumi wananchi wa wilaya ya Makete kwa ardhi yao kupangwa, kupimwa na kupata hati miliki ya ardhi ili kuendesha maisha yao ya kila siku kwa tija.
Lengo la kutekeleza mradi huo katika katika Halmashauri ya Makete na kusimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kutoa hati miliki za ardhi za kimila kwa wananchi wa halmashauri hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi ya Halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe Bw. William Makufwe hivi karibuni wakati anatoa tathmini ya utekelezaji wa mradi huo wilayani hapo.
“Naiona Makete mpya baada ya kukamilika Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ambao utawainua wananchi wa Makete kiuchumi, hawa ni wakulima na wafugaji. Sisi mkakati wetu ni kuendeleza wilaya hii, suala la kupanga, kupima na kutoa hati za kimila, kwetu ni kipaumbele na tunataka wananchi wetu wafanye shughuli zao za kiuchumi kisasa wakiwa na hati miliki za ardhi zao zitawafungulia fursa ya huduma za kibenki kwa shughuli za uchumi na kijamii” amesema Bw. Makufwe.
Wilaya ya Makete ina vijiji 98, kati ya hivyo, vijiji 28 vinanufaika na mradi wa LTIP huku vijiji 70 tayari ardhi yake imepangwa na kupimwa kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Hatua hiyo ya kila kipande cha ardhi kuwa katika mpango wa matumizi bora ya ardhi pamoja na wananchi kupata hati miliki itaifanya wilaya hiyo kuwa miongoni mwa wilaya ambazo ardhi yake ina thamani kubwa hatua inayowasaidia wananchi kupata dhamana katika taasisi za kifedha ikiwemo benki mbalimbali zilizopo wilayani humo ili kuongeza mitaji katika shughuli zao za kiuchumi.
Bw. Makufwe amesema mradi huo unapunguza migogoro ya ardhi kati ya kijiji na kijiji, wakulima na wafugaji, mkulima mmoja mmoja na jirani yake, wananchi na taasisi, wawekezaji na watumiaji wengine wa ardhi katika vijiji ili wananchi waendelee kutumia ardhi pasipokuwa na mitafaruku na mafarakano kwa kuwa wamehusishwa kupanga matumizi bora ya ardhi yao kupitia halmashauri ya kijiji pamoja mkutano mkuu wa kijiji.
Aidha, Bw. Makufwe ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuweka mazingira ya mazuri na rafiki ambayo ni chachu ya kupunguza changamoto za umilikishaji wa ardhi kwa wananchi kupitia mradi wa LTIP.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Msimamizi wa mradi wa LTIP wilayani Makete Bw. Enock Kyando amesema kulikuwa na migogoro ya ardhi 14 hadi sasa migogoro nane imetatuliwa huku migogoro sita bado inafanyiwa kazi kwa kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali ambapo wanatarajia hadi kukamilika kwa mradi huo migogoro yote ya vijiji itakuwa imetatuliwa.
Kwa upande wake Mweyekiti wa Mtaa wa Tandala wilayani Makete amesema mradi huo umekuja muda mwafaka na wameupokea vizuri kwa kuwa unamekuwa suluhisho la migogoro ya ardhi kwenye eneo lao kwa kuainisha matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya machungio, makaburi na viwanda vya kuchakata mbao hali ambayo haikuwepo kabla ya mradi huo na kila mtu atafanya kazi akiwa huru katika eneo lake kwa manufaa zaidi.
Naye Maria Sanga kutoka Kijiji cha Ikonda amesema si rahisi kijiji chao kuwa na migogoro mipya ya ardhi kwa sasa kwa kuwa ardhi yote imepangiwa matumizi kupitia mradi wa LTIP na migogoro iliyokuwepo inaendelea kutatuliwa na kupatiwa ufumbuzi kwa majadiliano ya pande zinazohusika kwa amani.