Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songwe CPA Cecilia Kavishe amesema Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) umetatua migogoro ya kimipaka katika halmashauri hiyo hatua inayowasidia wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali kwa amani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki Mkwajuni yalipo makao makuu ya halmashauri hiyo, CPA Kavishe amesema wananchi wa wilaya hiyo ni wakulima, wafugaji na wachimbaji wa madini, ujio wa mradi wa LTIP umesaidia kutatua migogoro ya mipaka kati ya wilaya ya Songwe mkoani Songwe na Chunya mkoani Mbeya ambao ulidumu kwa miaka nane tangu kuanzishwa kwa mkoa wa Songwe mwaka 2016.
"Ukiuangalia katika huu mradi hata ulipofika tu siku ya kwanza wakati tunautambulisha kwa wadau, kitu cha kwanza ambacho watu wengi walifurahia kwenye kile kikao ni kwamba tunaenda kutatua migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa ya wananchi pamoja na mipaka" amesema CPA Kavishe.
Akitolea mfano, CPA Kavishe amesema wananchi wa Kijiji cha Ileya wilayani Songwe wanafuraha migogoro imetatuliwa na mradi unaendelea kutekelezwa na hakuna mgogoro hata mmoja ambao umeshindikana kutatuliwa na kikosi ambacho kipo kazini.
CPA Kavishe ameongeza kuwa kuna ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa wilaya hiyo na timu inayotekeleza mradi huo inapotokea changamoto, uongozi wa wilaya unaweka nguvu na kasi ya kazi kuwa ya kuridhisha ambapo hadi sasa wanatarajia kugawa hati miliki za kimila 55 kati ya 75 kwa wananchi.
Aidha, CPA Kavishe amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huo umesaidia kutatua migogoro ambayo ilitakiwa kutumia gharama kubwa katika kupanga, kupima na kutoa hati miliki za ardhi kimila na kupima maeneo ya taasisi za Serikali hatua ambayo imepunguza gharama kwa halmashauri hiyo badala yake fedha ambazo zingetumika katika zoezi hilo sasa zimeelekezwa kutoa huduma za jamii kwa wananchi.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi wa LTIP Mkoa wa Songwe Bw. Remi Lipiki amesema hadi sasa wamefanikiwa kutatua mgogoro kati ya kati ya wilaya ya Songwe mkoani Songwe na Chunya mkoani Mbeya.
Migogoro hiyo iliyotatuliwa ni kati ya Kijiji cha Ileya kilichopo mkoa wa Songwe na Kijiji cha Lupa Market kilichopo wilaya ya Chunya mkoa wa Mbeya, Kijiji cha Ifwenkenya kilichopo mkoa wa Songwe na Kijiji cha Ipwizi kilichopo mkoa wa Mbeya, Kijiji cha Ifwenkenya kilichopo mkoa wa Songwe na Kijiji cha Mjele kilichopo mkoa wa Mbeya, Kijiji cha Ilasilo kilichopo mkoa wa Songwe na Kijiji cha Chang'ombe kilichopo mkoa wa Mbeya, Kijiji cha Patamela kilichopo mkoa wa Songwe na Kijiji cha Mwaoga kilichopo mkoa wa Mbeya na mgogoro kati ya Kijiji cha Itindi kilichopo mkoa wa Songwe na Kijiji cha Iyanga kilichopo mkoa wa Mbeya.
Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya Songwe Bw. Abraham Sambila amema mradi huo unawakomboa wana Songwe kumilikishwa ardhi kwa kupimiwa ardhi yake bure na kupewa hati.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa wanachi wakipata hati zao za umiliki wa ardhi wanaweza kuzitumia kukopa katika taasisi mbalimbali za fedha hatua inayowafanya wanufaike na ardhi yao na kufanya shughuli za kiuchumi kuboresha Maisha yao ya kila siku.