MPANGO WA MATUMIZI YA ARDHI KUCHOCHEA MAENDELEO NGARA
Imewekwa: 18 Apr, 2024
MPANGO WA MATUMIZI YA ARDHI KUCHOCHEA MAENDELEO NGARA

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) imeendelea na jitihada za kuhakikisha usalama wa milki za ardhi unaboreshwa ili kuchochea maendeleo ambapo kwa Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera takribani vijiji 75 vitanufaika na mradi huo kwa kupangiwa matumizi ya ardhi ambapo mpaka sasa vijiji 40 matumizi yake yamekwishaandaliwa.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwassa alipokuwa akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) wilayani Ngara tarehe 05 Aprili 2024 Mkoani Kagera.

 ‘‘Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya vijiji vyetu ni nyenzo ya upangaji inayoainisha matumizi mbalimbali ya rasilimali ardhi kulingana na mahitaji, hali halisi ya kiuchumi na kijamii, uwiano wa matumizi, ili kuongeza tija katika uzalishaji, uhifadhi na matumizi endelevu itasaidia katika kuongeza usalama katika milki za ardhi, kukuza huduma za kiuchumi na kijamii, kuboresha hifadhi ya mazingira na kumaliza migogoro itokanayo na ardhi’’ amesema Mwassa

Bi. Mwasa amesema kuwa ushirikishwaji unaofanywa hapa unatakiwa kwenda mpaka ngazi ya vijiji kila kiongozi katika eneo lake ahakikishe anasimamia utekelezaji wa mradi huu ikiwa lengo ni kuondoa malalamiko, migogoro ya ardhi pamoja na dhuluma kwa wananchi hivyo tuhakikishe ardhi ya watanzania inalindwa ili kuchochea maendeleo.

‘‘Kwa kupanga matumizi ya ardhi pamoja na kuishirikisha jamii itapelekea kumalizika kwa migogoro ya ardhi na kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Ngara’’ ameongezea Bi. Mwasa

Mkuu wa Wilaya ya Ngara Col. Mathias Julius Kahabi ameshukuru jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi huo Wilayani Ngara na kuahidi kuwa Wilaya ya Ngara itaendelea kushiriki katika utekelezaji wa mradi huu kwa manufaa ya wananchi wa Ngara.

Nae Afisa wa masuala ya kimazingira na kijamii Bi. Tumaini Setumbi amesema kuwa mradi huu umekusudia kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa kushirikiana na wananchi katika zoezi zima la upimaji na upangaji wa maeneo yao.

‘‘Mbali na mradi kutoa elimu kwa wananchi mradi huu umeendelea kuhamasisha umiliki wa ardhi kwa wanawake ikiwa ni pamoja umiliki wa pamoja baina ya mume na mke na kuzingatia haki za makundi maalumu’’ amesema Setumbi.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umedhamiria kuendelea kutoa elimu kwa wadau katika ngazi ya Kitaifa, Wilaya, Mtaa/Kijiji mpaka Kitongoji ambapo kupitia Mkutano huo wa Wadau katika ngazi ya Wilaya wadau watapata fursa ya kutoa maoni yao ili kuboresha utekelezaji wa mradi na kupelekea maendeleo katika maeneo yao.

Feedbacks

Mrejesho, Malalamiko au Wazo